Tuesday, 18 November 2014

NAMNA YA KUANZA SAFARI YA UTAJIRI - SEHEMU YA 2

2: chagua

Katika kila shilingi unayopata na kuishika mkononi una uhuru wa kuchagua mstakabali wako wa kuwa tajiri au masikini au mtu wa daraja la kati. Namna yako ya matumizi inaeleza wazi wazi wewe ni mtu wa namana gani. Kwa hiyo katika wakati huu ulio nao chagua kuwa tajiri. Na ukitaka kuwa tajiri jifunze namana ya kumiliki mali, mali ya kweli na sio ya kupita. Vijana wengi hurithi mali kutoka kwa wazazi wao na huipoteza bila kujua kwasababu hawajifunzi namna ya kuitunza, hivyo hata tukirithi mali bado tuna jukumu la kujifunza namna ya kuitunza na kuifanya iwe mali ya kweli.
Watu wengi huchagua kubaki masikini kutokana na kuwa na imani mbalimbali wengine husema “mimi sipendi hela”, “hamna shida mimi bado kijana bado nina muda”, “nikipata hela ya kutosha ndio nitafikiria nini cha kufanya”, “hamna shida mbona baba yangu ana fedha ya kutosha”. Mawazo kama hayo yanamfanya mtu afikie upeo wake wa kufikiri. Hata kama huna fedha jifunze juu ya kuzimiliki. Lakini bado tunabaki na uamuzi wa kuchagua kila siku; nini cha kufanya na muda wetu,fedha zetu,na nini cha kuwaza katika vichwa vyetu chaguo liko juu yetu. Na huo ndio uhuru wa kuchagua uhuru ambao kila mtu anao na ana wajibu wa kuutumia, uhuru wa kuchagua kuwa tajiri na tuna takiwa kuchagua kuwa matajiri kila siku ya maisha yetu.


WEKEZA KATIKA ELIMU;

Hakuna mtu anayeweza kukunyang’anya akili. Akili ndio mali pekee ambayo binadamu amejaliwa. Kila mtu ana uhuru wa kuchagua nini cha kuweka katika ubongo wake mala tu anapokuwa mtu mzima. Nyingi kati ya biashara zetu hufa kwasababu tunazianzisha kabla ya kujifunza namna ya kuendesha biashara. Hata leo hii naaandika kitabu kinachogusa maisha yetu ya kila siku lakini sijui ni watu wangapi watakihitaji na kukinunua badala ya kutumia fedha zao kununua pombe na CD za muziki na filamu. Wengi wetu tumeishia kununua TV na VCR,VCD, DVD n.k na ni wachache sana wanaonunua vitabu. Huo ndio uhuru wa kuchagua, ambao unabaki mikononi mwa kila mtu binafsi.

3: marafiki
Ushirikiano ndio nguzo ya mafanikio, utafanya ushirikiano na nani?. Hakika jibu litakuwa ni marafiki, ONYO, chagua marafiki na wala usiwachague kutokana na uwezo walio nao kiuchumi. Tuwe na marafiki, wawe mamilionea au mafukara nia hasa ni kujifunza kutoka kwao wote tena kwa ufahamu wa hali ya juu.
Namna yetu ya kujumuika na marafiki tajiri iwe ya makini wasije wakahisi kuwa tunajisogeza kwao kutokana na fedha walizo nazo. Inatakiwa tujifunze ufahamu walio nao kuhusu fedha. Na kuna pointi moja hapa naomba kuiongeza,watu wenye fedha maongezi yao huwa ya fedha na wala sikutanii ni kweli kabisa. Wao hufurahishwa na fedha wanatamani kuziongeza na sio kuzipunguza.kwa hiyo ukiwa na marafiki wenye fedha utajifunza kutoka kwao jinsi ya kupata fedha, kuziongeza na kuzitunza.
Na angalia marafiki ambao hawana fedha hawapendi kuongea kuhusu fedha, biashara wala uwekezaji. Na ukianza kuongea masuala ya fedha wakiwapo wanaona kama vile unaleta mikogo. Usiwaepe hao pia kwani kutoka kwao utajifunza usifanye nini kitakachokurudisha au kukuingiza katika ufukara. Hebu waulize marafiki zako wenye hela kama wana marafiki mafukara ambao wanafika kuuliza walifanya vipi kuukwaa utajiri, zaidi zaidi watakueleza mara nyingi marafiki wa namna hiyo wajapo kwao huja kwa nia hizi kama si zaidi ya hizi
 1. kuomba msaada
 2. kukopa 
 3. kuomba kazi.
Ni vema kutofuata ushauri wa watu masikini watu waliochanganyikiwa na maisha. Tusiwatenge ,tuwapende kwa dhati lakini inapofika masuala ya fedha au uwekezaji watakuambia biashara hii haitakulipa kuna watu wanawasikiliza na mambo yanawaendea kombo tatizo ni kwamba walisikiliza ushauri na kuufuata bila kudadisi kiundani na hawana sababu ya kulaumu wanapoanguka kwani wamesahau kuwa  “ndege wa mbawa moja huruka pamoja”. Unatakiwa kuwa makini sikiliza watu wote, fungua akili yako kwasababu unakuwa na mawazo yanayotofautiana na baada ya hapo utagundua yapi ni mawazo ya mtu tajiri na yapi ni ya mtu masikini.
Hakika jambo moja gumu kuwa tajiri ni kuwa mkweli kwa nafsi yako,na kujiepusha kufuata mkumbo yaani kufuata kile anachofanya kila mtu. Hebu fikiri juu ya dili linalotangazwa katika ukurasa wa mbele katika gazeti wao huita (front page) usilifuatilie umechelewa tafuta dili jingine, mlango mmoja unapofungwa mwingine unafunguliwa. Ukifuatana na marafiki matajiri utazijua dili kabla hazijafika “front page” kwa wafuata mkumbo, utajua mambo ya ndani kabla hayajafika nje na unapokuwa tayari umetengeneza faida ndio wengine wanaingia wakati wewe unatoka.

4: nini au nani anakuvutia.?

Kwa njia Fulani kuna mambo yanawezekana. Hivi ulipokuwa mdogo ni mtu gani ulipenda kuwa kama yeye (your child hero). Nilipokuwa mdogo nilipenda sana kuwa mwandishi wa vitabu kama Chinua Achebe, Ngugi Wa Thiong’o na James Hadley Chase. Kama watu niliojivunia nilijitahidi sana kusoma vitabu vyao kwa mfano nilijikuta nimesoma vitabu kama 25 vya Chase na nilivinunua kwa gharama yoyote ile hata ikibidi kutumia fedha yangu ya chakula shuleni. Nilihitaji kujua maisha ya watu hao, wametokea wapi mpaka kufika hapo walipo, kipato chao. Nilihitaji kujua kila kitu kuhusu wao kwasababu nilitaka kuwa kama wao.
Kutokana na hali hiyo nilitokea kuiongea lugha ya kingereza kwa ufasaha na kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa debate club shuleni. Wakati huo sikuwa mimi nilikuwa Chase, Ngugi na Chinua, lakini je hatimaye nilikuwa wao loh!! Niliwapoteza mashujaa wangu, heroes wangu kadili nilivyoendelea kuwa mtu mzima.
Leo hii waulize watoto wanataka kuwa kama nani… hapo  utasikia nataka kuwa kama Obama, Michael Jordan, Bill Gate, Lily Wayne,mwalimu Nyerere,Lady Jay D ( Judith Wambula), Erick Shigongo nk.Hawana kosa wanastahili kufanya hivyo kwani hiyo inawafanya kuwa na mtizamo kama watu hao maadamu tu wanaiga watu wale ambao wana mchango katika jamii unaotambulika na wa mfano bora wa kuigwa. Na ndio maana watu hao wakifanya jambo linaloikera jamii watu hupiga kelele sana kwani kufanya kwao maovu huwapotosha vijana wanaotamani kuwa kama wao.
Unafikiri itakuwa vema kwa mtu kama Erick Shigongo kuwa fisadi,hatutajisikia vibaya kwa yeye kupelekwa mahakamani tu bali atapoteza mashujaa wengi,vijana wanaojitahidi kuishi na kuwa kama yeye ghafra wanatakiwa kumsahau shujaa wao je unaufahamu msemo usemao “mti mkubwa unapoanguka huangukia miti midogo inayojitahidi kukua chini ya kimvuli chake” Sio kwamba kuwa hero kunakufanya uwavutie watu au kuwafurahisha tu hapana bali unafanya maisha kwao yawe rahisi kwani wakati wote watu watasema kama Reginard Mengi ameweza kwanini mimi nishindwe????. Inapofikia suala la kuanza biashara na kuwekeza watu wengi huona kama ni jambo gumu hilo lakini wanaona inakuwa rahisi wanapowafikilia mashujaa wao.


5: tunapata kuliko tunavyotoa
Kuna nguvu Fulani iliyofichika kuhusu kutoa. Kuna kitu unapaswa kukifanya katika maisha yako yote ni kujitolea pale inapobidi. Wape watu fedha, muda, pamoja na ufahamu pale inapobidi. Kama unataka kitu basi toa kitu kwanza. Ukijikuta una uhitaji wa fedha hebu saidia vikundi vinavyotoa huduma kwa jamii bila faida. Toa kwanza kile unachohitaji  na ndipo utapata kwa mamilioni sio wewe unahitaji tu na wala hutoi. Watu wengi najua hawataweza kufanya hivyo lakini amini usiamini ni jambo ambalo hakika huwa lina jibu, tena jibu chanya sio hasi.
Kama unaona hilo ni gumu basi wewe bado una fikra za kimasikini, bado unawaza kama mtu masikini kwani watu masikini daima ni wabinafsi sana kuliko watu tajiri. Kama mtu ni tajiri basi ujue anafanya kitu katika jamii ambacho watu wanakihitaji. Hivi ni busara kweli kwenda TANESCO na kuwaambia mkinipa umeme nitawapa fedha sijui kama kweli utapata kama usipotoa fedha.
Ni kweli kwamba unaweza kufanikiwa ukiwa peke yako lakini utafanikiwa haraka na zaidi kama ukiwa na wengine.

Tutaendelea na sehemu ya 3













No comments:

Post a Comment